| Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Kagasheki |
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida na wenzake watano wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa tuhuma za kusambaza dawa feki za ARV’s na kujipatia Sh milioni 148 kwa njia ya udanganyifu.
Madabida na wenzake, walipanda kizimbani jana mbele ya Hakimu Mkazi Nyigulile Mwaseba na kusomewa mashtaka matano na Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro.
Kimaro alidai shtaka la kwanza, linamkabili mshtakiwa Madabida (Ofisa Mtendaji Mkuu), Seif Shamte (Mkurugenzi wa Uendeshaji), Simon Msoffe (meneja masoko) na mshtakiwa wa nne, Fatma Shango (mhasibu msaidizi) wa Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd.
Alidai washtakiwa hao, wanadaiwa Aprili 5, 2011 jijini Dar es Salaam waliisambazia Bohari Kuu ya Dawa kopo 7,776 za dawa bandia za ARV’s zenye mchanganyiko wa dawa ya stavudin 30mg +nevirapine 200mg+lamivudine 150mg.
Dawa hizo zilizotengenezwa Machi, 2011 na kuisha muda wake wa matumizi Februari, 2013 zilionyesha kuwa ni halali wakati si kweli.
Shtaka la pili kwa washtakiwa hao, wanadaiwa kuisambazia Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kopo 4,476 na shtaka la tatu wanashtakiwa kwa kujipatia Dola za Marekani 98,506.08 (sawa na Sh 148,350,156 za Tanzania kwa udanganyifu, baada ya kuonyesha kwamba fedha hizo ni malipo ya makopo 12,252 ya dawa hizo za ARV’s.
“Mheshimiwa hakimu, shtaka la nne linamkabili mshtakiwa wa tano, Sadick Materu na mshtakiwa wa sita, Evans Mwemezi ambao wanadaiwa kati ya Aprili 5 na 13, mwaka 2011 wakiwa maofisa wa Bohari Kuu ya Dawa, walishindwa kuzuia kosa kutendeka.
“Shtaka la tano, linawakabili washtakiwa wote, mnadaiwa katika kipindi hicho mlishindwa kutimiza wajibu na kuisababishia Bohari ya Dawa hasara ya Sh 148,350,156.48,” alisema.
Washtakiwa walikana kutenda makosa hayo, upande wa Jamhuri haukuwa na pingamizi kwa washtakiwa kupewa dhamana, isipokuwa waliiomba mahakama kuzingatia sheria kwa kuangalia thamani ya fedha wanazodaiwa kujipatia washtakiwa.
Hakimu Mwaseba, aliwataka washtakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini dhamana ya Sh 6,181,256 kila mmoja, wawe wafanyakazi wa taasisi inayotambulika na kila mshtakiwa anatakiwa kuweka fedha taslimu au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh 12,362,513.
Washtakiwa wote, walitimiza masharti ya dhamana na mahakama iliwakubalia hadi kesi yao itakapotajwa tena kwa sababu upelelezi haujakamilika.
0 comments:
Post a Comment