![]() |
| MwanaCCM hai kutoka Jamhuri ya Watu wa China |
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimepata ushindi mkubwa katika uchaguzi mdogo Kata ya Mrijo, Wilaya Chemba, mkoani Dodoma.
Katika uchaguzi huo uliofanyika juzi, mgombea wa chama hicho, Khamis Msakati, alishinda kwa kura 1,261 na kuwashinda vibaya wapinzani wake.
Akitangaza matokeo hayo juzi usiku, Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi huo, Khamis Mwande, alisema Msakati alipata kura hizo kati ya kura halali 2,430 zilizopigwa.
Katika uchaguzi huo, Msakati alifuatiwa na mpinzani wake wa karibu, Said Kibinda (CUF), aliyepata kura 904, Omary Guka (Chadema) kura 248, huku mgombea wa NCCR-Mageuzi, Awadi Msuka, akiambulia kura 17.
“Tulitangaza matokeo saa 2:15 usiku, baada ya matokeo yote kufika katika kituo cha kujumlishia katika Kijiji cha Mrijo Chini. Kulikuwa na vituo 19 katika vijiji sita vinavyounda Kata ya Mrijo.
“Kimsingi tunashukuru uchaguzi umefanyika vizuri tangu kipindi cha kampeni hadi juzi tulipopiga kura hapakuwa na vurugu zozote, tumesikia sehemu nyingine watu wamekatana mapanga, lakini hapa Mrijo hali ilikuwa shwari.
“Wagombea wote walikubali kusaini fomu ya matokeo, ingawa mgombea wa NCCR-Mageuzi hakuweza kusaini, kwani aliingia mitini mwenyewe baada ya kuona ameshindwa vibaya,” alisema.
Kwa mujibu wa Mwande, wananchi waliotarajiwa kupiga kura katika kata hiyo walikuwa 7,434, lakini waliojitokeza walikuwa 2,448. Kura 18 kati ya hizo ziliharibika.
“Kwa takwimu hizo utaona takriban watu 5,000 hawakujitokeza kupiga kura. Sababu yake ni moja tu, huu ni msimu wa kilimo, watu wengi wapo mashambani,” alisema.
Msakati alisindikizwa kwa shamrashamra na nderemo kutoka eneo la ofisi za kata hadi nyumbani kwake, eneo la Chang’ombe, mara baada ya kukabidhiwa cheti cha ushindi.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Chemba, Al-haj Shaaban Kilalo, aliwashukuru wananchi wa Mrijo kwa kuendelea kuwa na imani na CCM na kusema kuwa hizo ni salamu kwa vyama vya upinzani.
Uchaguzi huo ulifanyika kujaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa diwani wa kata hiyo, Halifa Nyasuka (CCM), aliyefariki dunia Juni 15 mwaka jana, kutokana na maradhi ya kichwa.
Uchaguzi huo ni sehemu ya uchaguzi mdogo uliofanyika katika kata 27 nchini kote, kama ilivyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

0 comments:
Post a Comment