| Vijana wa Yanga wakiwa katika maandalizi ya kibano |
RAIS Jakaya Kikwete ameteuliwa kutoa mada katika mkutano maalumu wa kupambana na tatizo la ujangili duniani, unaotarajiwa kufanyika mjini London, Uingereza wiki hii.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema mkutano maalumu umeandaliwa na Mwanamfalme wa Uingereza, Prince Charles.
Alisema mkutano huo, utajikita zaidi kujadili tatizo la ujangili kwa wanyama kama tembo, faru na chui, ambao wamekuwa wakiuawa usiku na mchana.
“Rais Kikwete ameteuliwa katika jopo kubwa la viongozi kutoa mada juu ya tatizo la ujangili, hii ni heshima kubwa mno kwetu sisi ambao tumekuwa tunapambana na tatizo hili kila kukicha.
“Mkutano huu umekuja wakati ambao kuna vita kali ya ujangili wa tembo na faru, wanazidi kuuawa, tunaamini katika mkutano huu tutakuja na njia mpya ambayo itatusaidia kukabiliana na tatizo hili,” alisema Waziri Nyalandu.
Alisema juzi gazeti la Daily Mail la Uingereza liliandika habari za upotoshaji mkubwa kwamba Serikali ya Tanzania haijachukua hatua zozote za kukabiliana na ujangili.
“Tumesikitishwa na habari za upotoshwaji mkubwa uliofanywa na gazeti hili, eti linasema Tanzania haijafanya kazi yoyote ya kupambana na ujangili, nawahakikishia kazi imefanyika kwa nguvu kubwa mno, ninyi nyote ni mashahidi.
“Naomba ielewekwa kwamba shehena zote zilizokamatwa ndani na nje ya nchi ni juhudi za Serikali ikishirikiana na polisi wa kimataifa (Interpol), ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama.
“Tunapenda kuiarifu dunia kuwa katika kipindi cha kutoka mwaka 2010-13, jumla ya kilo 19,943, sawa na tani 20 za meno ya tembo zilikamatwa nchini, watuhumiwa 322 walikamatwa na kufikishwa mahakamni.
“Mwaka 2013 peke yake, tani 12.2 za meno zilikamatwa na watuhumiwa 145 walitiwa mbaroni, akiwamo raia wa Uingereza, Robert Dewar Twist, ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Trans Africa Logistic Limited ya Dar es Salaam,” alisema Waziri Nyalandu.
Alisema kwa takwimu hizo, ni wazi Serikali imeonyesha namna ambavyo inapambana vikali na tatizo hilo.
Alisema vita dhidi ya ujangili ni kali na ina mtandao mkubwa wa siri kutoka nje ya nchi, lakini Serikali imejipanga vya kutosha kukabiliana nao.
0 comments:
Post a Comment