Gazeti huru

Soma habari zenye uhakika
Home » » Jengo linalochungulia Ikulu kubomolewa

Jengo linalochungulia Ikulu kubomolewa

Written By Unknown on Friday, February 14, 2014 | 1:56 AM

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joesph Warioba
Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

MKURUGENZI Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Makumba Kimweri na Msanifu Mkuu, Richard Maliyaga wametiwa hatiani kwa kutumia madaraka vibaya, kwa kutoa kibali cha ujenzi wa ghorofa 18 jirani na Ikulu kinyume na utaratibu.

Mahakama imeamuru ghorofa kuanzia ya saba hadi ya 18, zibomolewe kwani haziko halali kutokana na matumizi ya eneo hilo.

Washtakiwa hao, walitiwa hatiani na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mjini Dar es Salaam jana mbele ya Hakimu Mkazi, Sundi Fimbo baada ya kupitia ushahidi na kuridhika kwamba washtakiwa walitenda makosa hayo.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Fimbo alisema washtakiwa walishtakiwa kwa makosa matano ya matumizi mabaya ya ofisi katika utoaji kibali cha ujenzi wa jengo la ghorofa 18 katika kiwanja namba 45 na 46 Mtaa wa Chimara.

“Mahakama imepitia ushahidi na kujiridhisha kwamba washtakiwa walitenda makosa hayo, hivyo wanatiwa hatiani kwa makosa yote matano.

“Mshtakiwa Kimweri, anatiwa hatiani kwa kosa la kwanza, la pili na shtaka la tano na mshtakiwa Maliyaga anatiwa hatiani kwa shtaka la tatu, nne na tano.

“Kutokana na mashtaka yanayowakabili washtakiwa, mahakama inawahukumu kwenda jela miaka mitatu kwa kila kosa au kulipa faini ya Sh milioni tano kwa kila kosa,” alisema.

Kutokana na hukumu hiyo, washtakiwa wanatakiwa kwenda jela miaka tisa na kulipa faini ya jumla ya Sh milioni 15.

“Jengo lilitakiwa liwe la ghorofa sita, hivyo mahakama inaamuru kuanzia ghorofa ya saba hadi 18 zibomolewe, naishangaa Manispaa ya Ilala kwanini haikuondoa ghorofa zilizozidi wakati sheria inawaruhusu,” alisema Hakimu Fimbo.

Hata hivyo, washtakiwa walinusurika kwenda jela baada ya kulipa faini waliyopangiwa na mahakama. Jengo hilo linamilikiwa kwa ubia kati ya Kampuni ya Royalle Orchard Inn na TBA.

Awali akiwasomea mashtaka, Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Leonard Swai alidai Agosti 6, 2007, Kimweri akiwa Mtendaji Mkuu wa TBA kwakutumia vibaya madaraka yake, alisaini hati ya makubaliano yenye namba TBA/JVA/DSM/ROI/001 kati ya TBA na Kampuni ya Royalle Orchard Inn Ltd, akiwa na lengo la kuanzisha ujenzi na wamiliki binafsi wa umma wa ghorofa 15, kwenye Kitalu namba 45 katika Mtaa wa Chimara, Wilaya ya Ilala bila eneo hilo kufanyiwa upembuzi yakinifu.

Alidai katika tarehe hiyo, Kimweri alitumia vibaya madaraka kwa kusaini hati ya makubaliano namba TBA/JVA/DSM/ROI/002 kati ya TBA na kampuni hizo akiwa na lengo la kuingia ubia kati ya Serikali na kampuni binafsi (PPP) wa ghorofa 15, kwenye Kitalu namba 46 eneo la Chimara bila kufanya upembuzi yakinifu katika mradi huo na kuipatia faida Kampuni ya Royalle Orchard Inn Ltd.

Alidai Julai 21, 2008, mshitakiwa Richard ambaye ni Msanifu Mkuu kwa kutumia vibaya madaraka yake, alitoa hati namba TBA/BP/155 na kuruhusu Kampuni ya Royalle Orchard Inn Ltd, kujenga ghorofa 15 za biashara kwenye Kitalu namba 45 na 46 bila ridhaa ya Mipango Miji ya Manispaa ya Ilala na kuipatia faida kampuni hiyo.

Pia alidai Aprili 9, 2009, Richard kwa kutumia madaraka yake vibaya, aliruhusu Kampuni ya Royalle Orchard Inn Ltd kujenga ghorofa 15 hadi 18 za biashara katika Mtaa wa Chimara, Kitalu cha 45 na 46 bila ridhaa husika ya Mipango Miji ya Manispaa ya Ilala na kuipatia kampuni hiyo faida.

Katika shtaka la mwisho, washtakiwa wote kwa pamoja walidaiwa katika tarehe tofauti katika ofisi za TBA, Kimweri akiwa Mtendaji Mkuu na Richard akiwa Msanifu Mkuu, katika utekelezaji wa kazi zao, walitumia vibaya madaraka kwa kuiruhusu Kampuni ya Royalle Orchard Inn Ltd kujenga jengo la biashara bila kupata ruhusa kwa ajili ya mabadiliko ya matumizi.
Share this article :

0 comments:

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. Jambo Leo - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger